15 Aprili 2025 - 22:10
Source: Parstoday
Wanachuo wa Iran waendeleza maandamano ya kuiunga mkono Palestina

Wanafunzi, maprofesa, wahadhiri na wafanyakazi wa Vyuo Vikuu vya mikoa ya Ardabil na Khorasan Kusini wamefanya maandamano ya kulaani ghasia na jinai zinazoendelea kufanywa na utawala wa Kizayuni wa Israel huko Gaza.

Katika Chuo Kikuu cha Mohaghegh Ardabili siku ya Jumatatu, Hojjatoleslam Abdollah Hassani, mwakilishi wa Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullah Sayyid Ali Khamenei alionyesha mshikamano wake na watu wa Gaza, na kuutaja mkusanyiko huo ni fursa ya kutetea wanaodhulumiwa na kuunga mkono mrengo wa Muqawama.

"(Mkusanyiko wa leo) unaadhimisha nembo ya kufichuliwa kwa ukandamizaji wa utawala wa Israel, na ahadi ya Mwenyezi Mungu kuhusu kusambaratishwa kwa utawala huu itatimia," Hojjatoleslam Hassani alisema wakati wa maandamano hayo.

Wakati huo huo, katika Chuo Kikuu cha Birjand, wanafunzi walikusanyika kwenye Msikiti wa Imam Jafar Sadiq na Haram ya Mashahidi Wasiojulikana, wakipiga nara kama vile "Mauti kwa Israeli". Waandamanaji hao wametaka kukomeshwa mara moja kwa jinai dhidi ya Wapalestina huko Gaza.

Mikusanyiko yote miwili ilihitimishwa kwa kusomwa kwa taarifa za kulaani vitendo vya Israel, huku washiriki wakithibitisha uungaji mkono wao kwa Palestina na harakati za Muqawama.

Maandamano hayo yanaonyesha hasira inayoongezeka nchini Iran kuhusu vita vya Gaza, huku vyuo vikuu kote nchini vikiendelea kuandaa maandamano kama hayo kwa ajili ya kuonyesha mshikamano na Wapalestina.

Israel imeua zaidi ya Wapalestina 1,600 tangu ilipoanzisha tena kampeni ya mauaji ya kimbari Gaza mnamo Machi 18, baada ya kuvunja makubaliano ya usitishaji vita wa miezi miwili uliokuwa umeleta utulivu kwa kiasi fulani katika eneo hilo.

342/

Your Comment

You are replying to: .
captcha